Search your Topic here

Friday, June 10, 2016

BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2016/2017

SERIKALI imewasilisha Bajeti ya Mwaka wa
Fedha 2016/2017 ya Sh trilioni 29.53,
ambayo nguvu kubwa imewekwa katika
kukusanya mapato kwa kulinda viwanda vya
ndani na kubana matumizi ya serikali ili
kuelekeza sehemu kubwa ya matumizi katika
maeneo ya vipaumbele.
Katika bajeti hiyo, bidhaa za lazima
zinazogusa maisha ya wananchi ikiwemo
mafuta ya petroli na dizeli pamoja na ushuru
wa barabara na maji ya kunywa, havijaguswa
huku bidhaa za starehe kama bia, sigara,
soda, juisi na nyingine kama nguo za
mitumba, huduma za kupanga nyumba na
uhamishaji fedha kwa simu, vikipandishwa
kodi, huku kiinua mgongo cha wabunge,
kufutiwa msamaha wa kodi.
Aidha, makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi,
ikiwemo mapato ya taasisi za udhibiti kama
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na
Mafuta (EWURA), Shirika la Viwango (TBS),
Jeshi la Polisi (Trafiki) na mamlaka nyingine
za udhibiti, sasa yatapelekwa moja kwa moja
katika Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo
mahitaji yao ya fedha yatatolewa na Wizara
ya Fedha na Mipango, badala ya kujigawia
kutokana na bakaa ya mapato
waliyokusanya.
Aidha, maduka ya kutoa huduma katika
majeshi, yamefutiwa kodi rasmi na badala
yake, Serikali inajipanga kuongeza posho
kwa askari, ili iwasaidie kukidhi mahitaji yao,
huku taasisi za umma na ofisi zote za
Serikali, zikipigwa marufuku kufanya
biashara na mzabuni asiyetumia mashine za
kodi za kielektroniki (EFD’s).
Kodi juu

Katika bidhaa zilizoongezewa ushuru na kodi
ni pamoja na vinywaji baridi, kutoka Sh 55
kwa lita mpaka Sh 58, huku ushuru wa
forodha katika maji ya matunda (juisi)
yanayotumia matunda yanayozalishwa hapa
nchini, ukipanda kidogo kutoka Sh 10 mpaka
11 kwa lita. Juisi zinazotokana na matunda
ambayo hayazalishwi hapa nchini, ushuru
wake pia umepanda kutoka Sh 200 kwa lita
hadi Sh 210 kwa lita.
Bia, vilevi, mvinyo
Kwa upande wa bia, serikali imependekeza
bia inayotokana na nafaka ya hapa nchini,
ambayo haijaoteshwa kama kibuku, ushuru
upande kutoka Sh 409 kwa lita mpaka 430.
Bia zingine, ushuru wake pia umepanda
ambao sasa utatoka Sh 694 mpaka 729 kwa
lita, huku bia zisizo na kilevi, ikiwa ni
pamoja na vinywaji vya kuongeza nguvu,
ushuru ukipanda kutoka Sh 508 kwa lita
mpaka Sh 534.
Kwa upande wa mvinyo uliotengenezwa kwa
zabibu zilizolimwa nchini kwa kiwango cha
asilimia 75, ushuru wake umepanda kutoka
Sh 192 kwa lita mpaka Sh 202.
Ushuru wa mvinyo unaotengenezwa na
zabibu zilizolimwa nje ya nchi kwa kiwango
kinachozidi asilimia 25 kutoka Sh 2,130 kwa
lita mpaka Sh 2,237. Vinywaji vikali,
havikuachwa nyuma maana ushuru
umepanda kutoka Sh 3,157 mpaka Sh 3,315.
Sigara
Sigara zisizo na kichungi zinazotengenezwa
kwa tumbaku ya hapa nchini kwa kiwango
angalau asilimia 75 kutoka Sh 11,289 hadi
Sh 11, 854 kwa kila sigara 1,000.
Kwa upande wa sigara zenye kichungi
zinazotengenezwa kwa tumbaku ya nchini
kwa angalau asilimia 75, ushuru juu kutoka
Sh 26,689 hadi Sh 28, 024 kwa kila sigara
1,000.
Sigara zenye sifa tofauti na hizo, ambazo
hazina vigezo hivyo vya tumbaku ya ndani,
ushuru wake umepanda kutoka Sh 48,285
hadi Sh 50,700 kwa kila sigara 1,000.
Katika tumbaku ambayo iko tayari
kutengenezwa kuwa sigara, ushuru wake
umeongezeka kutoka Sh 24,388 hadi Sh
25,608 kwa kilo huku ushuru wa sigara aina
ya Sigar ukibaki kuwa asilimia 30.
Vilainishi, gesi asilia, simu juu
Katika mafuta ya kulainisha mitambo, ushuru
umepanda kutoka Sh 665.50 kwa lita hadi Sh
699 kwa lita, huku ushuru wa grisi za
kulainisha mitambo, ukipanda kutoka senti
75 kwa kilo, hadi senti 79 kwa kilo.
Gesi asilia pia ushuru umepanda kutoka
senti 43 kwa futi za ujazo mpaka senti 45
kwa futi za ujazo.

Kuhusu viwango vya ushuru wa kuhamisha
fedha kwa kutumia simu, serikali
imependekeza kutoza ushuru wa asilimia 10,
kwenye ada zinazotozwa na watoa huduma
wa simu, katika kutuma na kupokea fedha,
badala ya ushuru huo kutozwa tu katika
kutoa fedha.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, kwa utaratibu
wa sasa, baadhi ya kampuni zinazotoa
huduma zimetumia mwanya wa kuhamisha
sehemu kubwa ya ada hizo kwenye kupokea
fedha na hivyo kuwa nje ya wigo wa kodi.

Ulaji wa wabunge, hisa
Kwa upande wa kiinua mgongo cha wabunge
wakati wa kustaafu, sasa kitatozwa kodi kila
mwisho wa muhula wa miaka mitano ili
kujenga misingi ya usawa na haki katika
utozaji wa kodi kwa kila mtu anayestahili
kulipa.
Aidha, mapato yote yatokanayo na hisa
katika kampuni mbalimbali sasa yatatozwa
kodi, baada ya kufutwa kwa msamaha kwa
waliokuwa wakimiliki hisa chini ya asilimia
25.

Kodi ya mishahara
Katika kodi inayokatwa katika mishahara
(P.A.Y.E), imepunguzwa kutoka asilimia 11
mpaka tisa kwa wafanyakazi wanaopata
mshahara wa kuanzia Sh 170,000 lakini
hauzidi 360,000. Kwa wanaopata zaidi ya
360,000 lakini haizidi 540,000, watakatwa Sh
17,100 pamoja na asilimia 20 ya kiasi
kinachozidi Sh 360,000.
Kabla ya hapo walikuwa wakikatwa Sh
20,900 na asilimia 20 ya kiasi kinachozidi Sh
360,000.
Wanaopata zaidi ya Sh 540,000 lakini haizidi
Sh 720,000, watakatwa Sh 53,100 pamoja na
asilimia 25 ya kiasi kinachozidi 540,000.
Kabla ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh
56,900 na hiyo asilimia 25 ya kiasi
kilichozidi 540,000. Kwa wanaopata zaidi ya
Sh 720,000 wao watakatwa Sh 98,100
pamoja na asilimia 30 ya kiasi kinachozidi
Sh 720,000.
Kabla ya hapo, walikuwa wakikatwa Sh
101,900 pamoja na asilimia 30 ya kiasi
kilichozidi Sh 720,000.

Kodi za nyumba
Serikali pia imependekeza malipo ya kupanga
nyumba, nayo yatozwe kodi ambayo
haikuweka kiwango, ila imependekeza
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato,
apewe mamlaka ya kukadiria kiwango cha
chini na cha juu cha mapato yapatikanayo
na pango ili yatozwe kodi.
Kodi za nyumba, usajili magari, pikipiki
Mbali na mapato ya kodi za nyumba, Serikali
imependekeza kupandisha ushuru wa kusajili
magari na pikipiki kutoka Sh 150,000 hadi Sh
250,000 kwa kila gari na kutoka Sh 45,000
hadi Sh 95,000 kwa kila pikipiki.
Kwa watumiaji wa namba binafsi za magari,
ada sasa itapanda kutoka Sh milioni 5 kila
baada ya miaka mitatu mpaka Sh milioni 10.

Kodi ya majengo
Aidha, kodi za majengo sasa hazitakusanywa
na halmashauri, badala yake TRA ndiyo
inayopewa mamlaka hayo ya kukadiria,
kukusanya, kuhifadhi na kuiwakilisha katika
halmashauri husika.
Mbali na TRA kupewa mamlaka ya
kukusanya kodi ya majengo, serikali pia
imependekeza kupunguza misamaha ya kodi
za majengo ili majengo mengi zaidi
yaingizwe katika orodha ya kulipa kodi.
Ulindaji wa Viwanda
Saruji aina ya (HS Code 2523.29.00)
zinazotoka nje ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ushuru wake wa forodha
umepandishwa kutoka asilimia 25 mpaka
asilimia 35 ili kulinda saruji inayozalishwa
nchini dhidi ya ushindani wa bei ya saruji
kutoka nje ya nchi.
Kwa bidhaa za chuma ikiwemo mabati
kutoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,
nazo ushuru umetoka asilimia 0 mpaka 10,
ili kulinda uzalishaji wa bidhaa hizo hapa
nchini, huku bidhaa za nondo kutoka nje
nazo zikipandishwa kodi kutoka asilimia 10
mpaka 25, kwa nia ya kulinda viwanda vya
ndani.
Nyavu za kuvua samaki kutoka nje ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki, ushuru wake
umepanda kutoka asilimia 10 hadi asilimia
25 huku vichujia vya vilainishi na petroli
kutoka nje ya nchi vikiongezwa ushuru
kufikia asilimia 25 kutoka asilimia 10, ili
kulinda bidhaa za ndani.
Sukari, ngano, mitumba, mafuta ya kula
Katika sukari, serikali imekusudia kupunguza
msamaha wa kodi na hivyo waagizaji wa
bidhaa za sukari kutoka nje watalazimika
kuanza kulipa ushuru wa asilimia 15 kutoka
asilimia 10, huku ikitarajiwa kuongezeka
zaidi na kuwa asilimia 20 mwaka 2017/18
na asilimia 25 mwaka 2018.19, ili kulinda
viwanda vya ndani.
Kwa upande wa ngano kutoka nje, ushuru
umepunguzwa kutoka asilimia 35 mpaka 10,
kwa kuwa nchi za Afrika Mashariki hazina
uwezo wa kuzalisha kulingana na mahitaji.
Kwa upande wa nguo na viatu vya mitumba
Serikali imepandisha ushuru kutoka dola za
Marekani 0.2 mpaka dola za Marekani 0.4
kwa kilo, kwa nia ya kudhibiti nguo hizo
lakini pia imetangaza kujiandaa kuzuia
uingizaji wake.
Kwa upande wa mafuta ya kula kutoka nje
nayo ushuru umepanda kutoka asilimia 0
mpaka 10 kwa mafuta ghafi ya kula, ili
kuimarisha kilimo cha mbegu za mafuta na
viwanda vya ndani.
Tozo za pamba, kahawa, korosho
Miongoni mwa tozo zilizofutwa kuondoa kero
kwa wananchi ni mchango kwa kila kiwanda
cha kuchambua pamba wa Sh 450,000 na
ada ya vikao vya halmashauri wakati wa
kujadili wafanyabiashara wa pamba ya Sh
250,000.
Kwa upande wa kahawa, Serikali imefuta ada
ya leseni ya kusindika kahawa ya dola za
Marekani 250, huku ushuru wa kusafirisha
korosho wa Sh 50 kwa kilo, ukifutwa.
Tozo zingine zilizofutwa katika korosho ni
ushuru wa chama kikuu cha ushirika Sh 20
kwa kilo, gharama za mtunza ghala Sh 10
kwa kilo, kikosi kazi cha kufuatilia masuala
mbalimbali Sh 10 na makato ya unyaufu.
Pia Serikali imepanga kuendelea kufuta tozo
nyingine zinazokatwa na halmashauri,
wakala na mashirika katika mazao ya
wakulima, baada ya kufanya tathmini za
kina.

Maduka kambi za jeshi
Serikali imependekeza kufuta msamaha wa
kodi uliokuwa ukitolewa katika maduka na
migahawa maalumu kwa ajili ya askari wa
majeshi, kutokana na msamaha huo
kutumiwa vibaya na kupoteza mapato ya
serikali na badala yake, askari watapata
posho mpya juu ya posho ambazo
wamekuwa wakipewa.

No comments:

Follow us